Mwakyembe: Ntahakikisha Nawapata Waliomteka Roma ili Kukomesha Tabia Hii
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesikitishwa na vitendo walivyofanyiwa wasanii wa muziki Roma Mkatoliki na wenzake huku akisema hawezi kukubali kuona mambo kama hayo yakiwa yanaendelea kutokea.
Akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam, Waziri huyo amesema kilichotokea siyo hali ya kawaida kwa watanzania kamwe hawezi kukubaliana na jambo hilo huku akisisitiza kuwa atafuatilia kwa ukaribu sana ili aweze kupata majibu ya haraka kabla hajawasilisha bajeti ya wizara yake
"Hiki kilichotokea siyo hali ya kawaida kwa watanzania, hatuwezi kukubali kitu kama hiki kiendelee kutokea,nitalifuatilia kwa ukaribu sana, nitajitahidi nipate majibu kabla ya bajeti yangu Bungeni". Alisema Dk. Mwakyembe
Hata hivyo Dkt. Mwakyembe amewataka wananchi waache tabia ya kuamini kila maneno yanayosemwa na watu ambao hawana ujuzi katika masuala ya uchunguzi, hivyo wanapaswa kuvipa muda vyombo vya dola viweze kufanya kazi zake kwa ufasaha.
"Nilishasema kuwa nimeagiza vyombo vya dola vifanye uchunguzi ili ajulikane aliyewafanyia hivi wakina Roma kama ni nani kama wa dola ntadili naye, tuache uchunguzi ufanyike, tuache kupiga ramli". Alisisitiza Mwakyembe
Pia Waziri huyo mwenye dhamana na wasanii ametoa ujumbe kwa vyombo vyote vilivyopo chini ya Wizara yake kutofanya mahojiano yoyote yanayowahusu wasanii hao bila ya kuwepo taarifa kamili kutoka kwake.
Kwa upande mwingine Roma ambaye ambaye amesimulia tukio lilivyokuwa amesema kwa sasa hawezi kuongea mambo mengi kwa kuwa kila kitu amekwisharipoti polisi kila kitu, na kwamba kuna mambo akiyaweka hadharani atakuwa anaingilia upelelezi wa polisi.
Pia amesema hawezi kujua kama kweli tukio hilo lililowatokea linahusiana na muziki kwa kuwa ameweza kuhusishwa mpaka mfanyakazi wao wa ndani ambaye hana hata chembechembe za uimbaji.
Post a Comment